JINSI YA KUTUNZA WANJA WA PIKO


BAADA ya teknolojia kuzidi kuongezeka kila siku, imefanya na masuala
ya urembo pia kuendelea.

Hapo zamani sana, mwanamke alikuwa akitumia kujipaka wanja kwa njiti
iliyoungua, ama makaa nakadhalika, wanja ambao ulikuwa haudumu muda
mrefu katika nyusi. Lakini siku hizi kuna wanja za aina mbalimbali
ikiwemo wanja wa piko na tatuu.

Wanja wa piko umekuwa ukidumu kwa masiku kadhaa usoni, na kuondoa
usumbufu wa kupaka wanja kila siku, hali ambayo inarahisisha katika
suala la kujipamba hususan uso.

Sasa, ili wanja huo uweze kudumu kwa muda mrefu, ni vyema baada ya
kupaka ukakaa nao muda mrefu na wakati wa kubandua magamba
yanayojiweka juu baada ya kukauka ukatumia mafuta.

NIA YA HII PICHA NI KUONYESHA WANJA WA PIKO NA SI VINGINEVYO

Haya tuendelee...

Kisha, kila asubuhi hakikisha unapitisha wanja wa kawaida tena
itapendeza zaidi ukipitisha wa rangi ya hudhurungi, na wakati wa
kunawa ama kuoga angalia usisugue sana sehemu ya nyusi.

Utumiaji wa wanja huu utakurahisishia na kupunguza muda wako wa kukaa
mezani, lakini pia utakufanya kuwa marudadi muda wote usoni.

Ni vizuri kama utaenda kupakaliwa saluni,  kwa kuhofia kujiharibu
lakini pia kama utakuwa unajimudu kujipaka nyumbani basi chukua piko
robo kijiko cha chai kisha weka kwenye kikopo au kisahani halafu tia
maji kidogo sana kisha unakoroga mpaka uhakikishe unakuwa mzito saizi
ya kati.

Baada ya hapo chukua kioo na kiwembe sawazisha nyusi zako kwa kuzinyoa
mtindo uupendao, kisha paka kwa kufuata ulivyoa nyusi.

Tulia kwa muda wa dakika 20 hadi 30 mpaka ukauke vizuri kabisa, baada
ya muda huo, paka mafuta ya mgando juu ya nyusi ili kulainisha na
kutoka kwa wepesi, na utaona magamba yanatoka kufuata mchoro wa wanja.

Waweza kwenda oga sasa na kuendelea na vipodozi vingine, kwa kawaida
wanja huu hudumu wiki moja lakini ukiutunza vizuri unaweza kudumu
zaidi ya hapo.

No comments:

Post a Comment