Hereni...nakshi tamu kwenye urembo


HERENI ni moja kati ya pambo muhimu kwa mwanamke, na pambo hili ni
maalum kwa ajili ya sikio.

Japo huwa ni maalum kwa ajili  ya mwanamke, lakini wapo pia wanaume wanaovaa, ingawa sitawazungumzia hapa.

Hereni kama ilivyo ada, pambo hili kuvaliwa masikioni, likiwa limenakshiwa
katika mitindo mbalimbali kulingana na matakwa ya  mvaaji.

Kuna hereni kubwa, ndogo, saizi ya kati na za kila rangi, pia zipo za maua pamoja na maumbo mbalimbali kama vile msalaba, nyota na mwezi, kipepeo, kiatu na nyingine nyingi.


Karibu wanawake wote wanafahamu pambo hili, na kwa kuonesha umuhimu wake, hata wale ambao hawajatoga masikio, pia huvaa za kubana (maalum kwa ajili yao).

Uzuri wa pambo hili linapatikana kwa kila bei, kuna hereni za asili, dhahabu, almasi na madini tofauti tofauti na pia malighafi tofauti, hivyo uamuzi wa mvaaji hutokana na kipato chake.

Pamoja na kwamba pambo hili ni maarufu lakini nalo pia lina kanuni zake katika uvaji, kwa mfano mtu mwenye sura nyembamba au ndogo hapendezi akivaa hereni kubwa kupita kiasi, pia vile vile
katika mpangalio wa rangi, kwani unaweza kuvaa hereni nzuri lakini kutokana na mpangilio mbaya wa rangi ukaonekana kituko.

Hereni huongeza umaridadi mara dufu kwa mwanamke,  na ni vyema ukachagua rangi mahsusi kulingana na nguo uliyovaa au mapambo ya mwili, na ukizingatia hilo, ama hakika utakuwa ni maridadi na wa kuvutia.

Angalia pia aina ya uso wako, kama ni duara waweza vaa hereni saizi kubwa kiasi, na ni vyema unapovaa hereni angalia na mtindo wa nywele. Kama nywele zinaficha masikio basi ni vizuri kama utavaa
hereni zenye kuonekana ambazo ni kubwa kiasi.



Hakikisha una aina tofauti tofauti za hereni ambapo utapata urahisi katika kuchagua nguo, mapambo ya mwili na viatu.

Kama una lolote fadhali ongezea, kupitia rabia.bakari@gmail.com..facebook utanipata kwa jina la  classic rabia....Karibu sana

No comments:

Post a Comment