Jinsi ya kutunza uso


KATIKA mwili wa binadamu, kitu cha kwanza muhimu katika muonekano ni uso, na ndio maana wanawake wengi wamekuwa na msemo 'mapokezi kwanza', wakimaanisha umaridadi wa uso na kisha
vingine vinafuatia.

Basi pamoja na umuhimu huo wa uso lakini wengi wetu hatujui namna ya kuutunza hata uwe wenye kuvutia kila siku, na badala yake tumekuwa tukifanya kwa mazoea kwamba baada ya kunawa ama kuoga unapaka mafuta na vipodozi, umemaliza.



Wanaodhani hivyo, wanakosea sana, uso unahitaji matunzo mazuri na unahitaji uangalizi wa hali ya juu,  kwani ndio uhalisia wako kabla ya kuonesha mapambo mengine.

Kwanza ni vizuri kama utakuwa ukiosha uso wako kwa maji safi na salama, kwani kwa kufanya hivyoutasaidia kupenuka bakteria wanaoweza kukudhuru katika ngozi ya uso.

Pia ni muhimu kupaka bidhaa inayoendana na ngozi ya uso wako, kwa mfano kama ngozi yako ina mafuta  pendelea kutumia maji ya uvuguvugu na bidhaa zenye limao kwa  ajili ya kupunguza mafuta, na pia chagua bidhaa kwa ajili ya ngozi yako.



Chagua sabuni sahihi kwa ajili ya kuoshea uso wako, usipende kutumia sabuni yoyote inayokuwa mbele yako,  kwani nyingine inaweza kukinzana na ngozi ikawa tabu, kwani ngozi ya uso ikiharibika huchukua
muda mrefu kurudi katika hali yake ya kawaida.

Tafuta taulo maalum kwa ajili ya uso, na hakikisha mara zote ni safi.  Pia kupumzika kwa muda unaotakiwa,  ni kitu muhimu sana, kufanya kazi nyingi bila kupumzika, huchosha ngozi ya uso na hata muda mwingine kuondoa nuru ukaonekana mtu mzima tofauti na umri.

Pumzisha ngozi ya uso usiku kwa kutopaka kipodozi chochote ama kulala na kipodozi ulichopaka mchana.

Epuka kukasirika mara kwa mara na kukunja uso, imarisha ngozi kwa ujumla, usile vyakula hovyohovyo, zingatia matunda, maji mengi, na mbogamboga, huku ukizuia uso kupigwa na jua  muda mrefu.

Si lazima kufanya dondoo zote hizi lakini ukifuata baadhi tu itakusaidia  na hakika utakuwa na uso wenye kuvutia.

No comments:

Post a Comment