Lucy azungumzia jinsi ya 'kuhandle' nguo chache

KINA dada wengi, husumbuliwa na suala la kuwa na nguo chache. Na wengine hufadhaika na kupata msongo wa mawazo hata kujishusha hadhi wawapo katika kundi au mkusanyiko wa watu.

Lakini mara nyingi hali hiyo hutokea kwa mtu ambaye hushindwa kuzipangilia nguo hizo chache alizonazo, na kujikuta akikosa nafasi ya kuwa huru pale alipo.

Kuwa na nguo chache kunaweza kuchangiwa na kukosa muda wa kwenda kutafuta kwa sababu mbalimbali kama vile kubanwa na kazi, masomo, majukumu ya nyumbani nakadhalika.

Lakini pia muda mwingine husababishwa na bajeti finyu, au kukosa nguo ambazo zinakukaa vizuri katika maduka au maeneo yanayouzwa nguo. Kwa mfano, mtu mwingine hupendeza akivaa nguo za silk, ama zenye kubana, wakati wengine nguo za mpira huwakaa vizuri zaidi na mfano kama huo.

Hii husababisha muhusika kupenda nguo chache ambazo amebahatika kuzipata, lakini pia inaweza ikamsumbua sana katika kuzipangilia hata kujisikia vibaya anapozirudia rudia na kuwaza huenda jamii inayomzunguka inamuona yeye wa hali fulani.

Lucy Gift, mwanadada wa kisasa na mtanashati mtanzania anayeishi Uingereza kwa sasa anaeleza kwanza alivyopata shida kipindi akiwa na nguo chache lakini anaeleza pia namna nzuri ya kupangilia nguo hizo hata ukajisikia vizuri na usione tofauti kubwa kati yako na wale walio na nguo nyingi.
Anasema ukiwa na nguo chache, na ukazirudia mara kwa mara ni wazi utajishtukia uwapo na marafiki zako, ama kazini na hali hiyo ilikuwa ikimkuta sana kipindi hicho.


Lucy Gift pichani

Lakini pia hata katika mitoko mbalimbali, maana unaweza ukajikuta unarudia nguo moja katika sherehe nyingi ama mikutano mbalimbali.

"Na suala hili huenda likakunyima raha ya kuwa huru uwapo na marafiki kwa kweli,"anaongeza.

Lakini anaelezea kuwa tatizo lingine kubwa, ni mtu kukumbuka kirahisi kwa sababu kwa yule ambaye
uliwahi kukutana nae mara moja mahali, nguo inakuwa alama nzuri sana kwake, na anasema mara nyingine inaweza kuwa bahati mbaya hata mtindo wa nywele ukawa ni ule ule ambao ulikuwa nao wakati ukikutana na mtu huyo.

Akielezea mbinu ya kufanya, anasema ukiwa na nguo chache suala kuwa ni kuzipangilia kinamna ili isiwe rahisi mtu kukugundua kuwa una nguo chache.

"Kwa mfano ukiwa na sketi zako kama nne hivi za mitindo na rangi tofauti hakikisha mojawapo iwe nyeusi na yenye hadhi fulani. Kwa sababu sketi nyeusi zinaendana na blauzi ya rangi yoyote,"anasema.

Ukishafanikiwa kuwa na sketi hizo, Lucy anasema unaweza kuongeza  blauzi angalau saba nzuri, ambazo zitafunika wiki nzima.Halafu unatakiwa kuchanganya changanya blauzi na sketi, usirudie sketi na blauzi moja, kama ulivyovaa wiki iliyopita.

"Chagua kwa makini mavazi yako kutokana na kazi unayofanya, ni muhimu sana, kwa hiyo una uwezo wa kubadili blauzi na sketi kila siku na watu wasikushtukie kirahisi tokana na vile unavyochanganya,"anasema.

Anakupa 'tip' nyingine kuwa baada ya hapo unaweza ukaongeza magauni kama manne hivi yenye mitindo tofauti likiwemo na la mtoko kwa ajili ya jioni.

"Bila kusahau, lazima uwe japo na gauni moja jeusi ambalo linaweza kukusaidia pale ukiwa katika hali inayohitaji kuwa na vazi lisilo na makuu...unakuwa umemaliza."

No comments:

Post a Comment